Baba mbaroni tuhuma za kumjeruhi mwanaye kichwani
Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia Amran Burhan, mkazi wa Mtaa wa Kilimani,Kata ya Pasua Manispaa ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za kumjeruhi kichwani mtoto wake wa miaka 14 kwa kutumia kitu chenye ncha kali.
Tukio hilo limetokea Oktoba 26, 2026, katika Mtaa wa kilimani, Kata ya Pasua, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo leo, Oktoba 29, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amesema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Jumatatu, Oktoba 26 ambapo uchunguzi unaendelea kubaini chanzo chake na kukusanya ushahidi kwa ajili ya hatua za kisheria. “Chanzo cha tukio hili bado kinachunguzwa ikiwa ni pamoja na kukusanya ushahidi ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe dhidi yake.” Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, mtoto huyo amepatiwa matibabu na kupelekwa katika nyumba salama kwa ajili ya uangalizi na ulinzi.
“Mtoto aliyeathirika na tukio hilo amepatiwa matibabu na kupelekwa katika nyumba salama kwa ajili ya uangalizi.” amesema Kamanda Maigwa.
Awali akisimulia tukio hilo kwa uchungu mtoto huyo alidai kuwa baba yake amekuwa akimpiga mara kwa mara akimtuhumu kuiba fedha nyumbani, kabla ya kumjeruhi kichwani na mkononi.
“Walikuwa wanasema nimeiba hela. Baba akawa ananipiga, akaniambia nilale chini. Alipochukua kitu kilichokuwa kwenye moto anichome nacho, nilikataa, nikakinga kwa mkono, akanichoma na kunikata kichwani utosini kwa kisu,” alisema mtoto huyo.
Mtoto wa miaka 14, mkazi wa Pasua, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, akionekana katika eneo la nyumba wanayoishi baada ya kudaiwa kufanyiwa ukatili na baba yake mzazi. Picha na Yesse Tunuka
Alidai baada ya tukio hilo, baba yake alimnyoa nywele na kumpaka dawa kichwani, ingawa hakufahamu aina ya dawa aliyotumia.
Mtoto huyo pia alisema alikuwa akiishi kwa hofu kutokana na vipigo vya mara kwa mara alivyodai kufanyiwa, ikiwemo kwa sababu ya migogoro na watoto wengine wa baba yake.
Alikaa nje ya shule miaka mitatu
Inadaiwa kuwa mtoto huyo awali alikuwa akiishi na bibi yake na kusoma katika Shule ya Msingi Ntomoko, iliyopo Kata ya Haubi, Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma.
Mwaka 2023, alipokuwa darasa la nne, bibi yake alifariki dunia na kumlazimu kwenda kuishi na mama yake mzazi katika kijiji kingine mkoani humo.
Hata hivyo, hakuendelea na masomo baada ya kuhamia kwa mama yake na taratibu za uhamisho wa shule hazikufuatiliwa, ambapo kama angeendelea na masomo mwaka huu angekuwa anamaliza darasa la saba.
Alisema baba yake, Amran Burhan, aliyekuwa akiishi Moshi, alianza kumpigia simu mama yake na kumtaka aende kuishi naye, akieleza kuwa tangu azaliwe hawakuwa wamewahi kukutana ana kwa ana hadi alipofika Moshi.
“Baba ndiye aliyeanzisha mawasiliano na mama kwamba nije Moshi, mama hakuwa na shida yoyote labda ya kunitesa,” alisema.
Mtoto huyo alisema baada ya kufika Moshi, alianza kukumbana na matatizo nyumbani kwa baba yake. Alidai mawasiliano yake na mama yake yalikatika baada ya baba yake kuchana karatasi aliyokuwa ameandika namba ya simu ya mama yake, akimtuhumu kumpelekea taarifa za mambo yaliyokuwa yakitokea nyumbani.
“Nisaidie tu nirudi kwa mama yangu nikaendelee na masomo,” alisema.
Kwa upande wake, Joyce Swai, mwenye nyumba inayoishi familia hiyo, alisema hakushuhudia tukio la mtoto kupigwa, lakini alifahamu kuhusu jeraha lake baada ya kuzungumza naye.
“Nilimkuta kakaa nje asubuhi ana jeraha nilipomuuliza akasema aliyemkata ni baba yake akimtuhumu kuiba hela na amepigwa mpaka akachanwa kichwa,” alisema Joyce. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limewataka wananchi kutoa taarifa wanapobaini vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi, likisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kuhusika.
