Rais Mwinyi akutana na kampuni za Korea, kuvutia uwekezaji Zanzibar
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, amekutana na viongozi wa taasisi na kampuni za Korea Kusini kujadili fursa za ufadhili na uwekezaji wa mabilioni ya fedha kwa ajili ya miradi ya kimkakati ya maendeleo Zanzibar.
Mikutano hiyo imefanyika leo Ijumaa, Oktoba 30, 2026, jijini Seoul, na viongozi wa K-FINCO, HEERIM, Sejong Plant, Samoo C.M. Architects & Engineers pamoja na Sung Shin Rolling Stock Technology Ltd (SSRST).
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zanzibar, mazungumzo hayo yamejikita katika maeneo ya usafiri wa baharini, bandari, barabara, miundombinu ya mijini, nishati mbadala, utalii, viwanda na afya.
Taarifa hiyo imesema taasisi ya kifedha ya K-FINCO imeeleza mifumo mbalimbali ya dhamana na ufadhili inayotumika kuwezesha kampuni za Korea kushiriki katika miradi ya maendeleo ya Zanzibar.
Kwa upande wa miradi ya afya na utalii wa mikutano, kampuni ya HEERIM imetangaza kuwa tayari imeandaa mpango wa maendeleo ya mradi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano na Maonesho Zanzibar (MICE), huku taratibu za kumpata mshauri elekezi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni zikiendelea.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi (wa pili kushoto), akizungumza na baadhi ya viongozi wa kampuni kubwa za Korea Kusini.
Rais Dk Mwinyi amesema mradi wa Hospitali ya Binguni utahusisha sio tu huduma za afya, bali pia mafunzo, hivyo unahitaji vifaa tiba vya kisasa, mifumo bora ya taarifa za hospitali na utaalamu wa hali ya juu wa usanifu na usimamizi, ambapo kampuni ya SAMOO C.M na washirika wake wamewasilisha uzoefu wao katika maeneo hayo.
Katika sekta ya maji, mazingira na uchumi wa buluu, kampuni ya Sejong Plant imeonyesha nia ya kushiriki katika miradi ya maji safi na salama na usafishaji wa maji taka, pamoja na kuangalia njia za ufadhili.
“Kampuni hiyo pia imeonesha nia ya kuagiza mazao ya uvuvi kutoka Zanzibar na kuwekeza katika mifumo ya uhifadhi kwa baridi ili kusaidia upatikanaji wa soko na kulinda ubora wa mazao hayo,” imesema taarifa hiyo.
Sambamba na hayo, Rais Mwinyi ameeleza mpango wa Serikali wa kurejesha huduma ya reli ya abiria na utalii Zanzibar, ambapo kampuni ya Sung Shin Rolling Stock Technology Ltd imeonesha nia ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mradi huo wa kihistoria.
Rais Dk Mwinyi amesisitiza kuendelea kwa mawasiliano ya kitaalamu ili kuchambua miradi iliyojadiliwa, mahitaji yake na mifumo inayowezekana ya ufadhili, kwa kuzingatia taratibu za Serikali na sheria za zabuni.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, akizungumza na baadhi ya viongozi wa kampuni kubwa za Korea Kusini nchini humo
Baada ya mikutano hiyo ya moja kwa moja na kampuni, Rais Dk Mwinyi alikutana na jumuiya ya wawekezaji na wafanyabiashara wa Korea Kusini katika hafla ya chakula cha jioni kilichoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, iliyofanyika katika Hoteli ya Grand Hyatt, jijini Seoul.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na wawakilishi wa Serikali ya Korea Kusini, wanadiplomasia, viongozi wa taasisi za fedha na wawekezaji, Dk Mwinyi amewakaribisha wawekezaji wa Korea Kusini kutumia fursa za uwekezaji Zanzibar na kushirikiana na wafanyabiashara wa ndani ili kuongeza mitaji na kuleta teknolojia mpya.
“Zanzibar ina fursa nyingi za uwekezaji, hususan katika sekta za Uchumi wa Buluu, utalii, bandari, usafirishaji na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, ambazo zimepewa kipaumbele katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050,” amesema Rais Mwinyi.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kupitia sheria na kanuni zinazolinda maslahi ya wawekezaji, pamoja na kuimarisha huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), ili kurahisisha uanzishaji na uendeshaji wa miradi.
Amesema Zanzibar ina nafasi nzuri ya kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji kutokana na eneo lake la kimkakati linalounganisha masoko ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, pamoja na fursa zinazotokana na Soko Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).
Rais Mwinyi amewahimiza wafanyabiashara wa Korea kuanzisha ubia na kampuni za Zanzibar, akieleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuunganisha uzoefu, teknolojia na mitaji kutoka Korea Kusini na fursa zilizopo Zanzibar kwa manufaa ya pande zote mbili.
Kwa mikutano hiyo, Rais Mwinyi amekamilisha ziara yake ya kikazi nchini Korea Kusini, iliyohusisha mikutano ya uwekezaji na biashara jijini Seoul, ziara za viwanda na miradi jijini Yeosu na ushiriki katika Mkutano wa ITOPF visiwani Jeju.

