Azimio la Dar lasisitiza ushawishi wa vijana kwenye mabadiliko ya tabianchi
4 mins read

Azimio la Dar lasisitiza ushawishi wa vijana kwenye mabadiliko ya tabianchi

Dar es Salaam. Vijana 61 kutoka nchi 17 za Afrika wamehitimu mafunzo ya majadiliano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi. Lengo likiwa kuongeza ushawishi wa vijana wa Afrika katika maamuzi yanayohusu mustakabali wa bara hilo.

Azimio hilo linaweka msisitizo katika kuhamisha ushiriki wa vijana kutoka kuhudhuria mikutano hadi kuwa na sauti yenye ushawishi katika majadiliano, haki ya tabianchi na maendeleo endelevu.

Limepewa jina la “Dar es Salaam Declaration on African Youth Climate Change Negotiations”, likiwa na kaulimbiu inayotafsiriwa: “Kutoka Ushiriki hadi Ushawishi: Kuwawezesha Vijana wa Afrika Kuathiri Majadiliano ya Tabianchi, Haki ya Tabianchi na Maendeleo Endelevu.”

Mafunzo hayo yalihitimishwa Oktoba 22, 2026, yakishirikisha vijana 61 huku 45 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na wengine wakitoka katika nchi nyingine za Afrika.

Akizungumza katika hafla ya kuhitimisha mafunzo hayo, Mtaalamu Mwandamizi wa Nishati, Mabadiliko ya Tabianchi na Udhibiti wa Majanga wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania, Dk Abbas Salum Kitogo, amesema lengo ni kuhakikisha vijana wanatumia maarifa waliyopata kuleta mabadiliko ya vitendo katika jamii.

Ametaja maeneo manne yanayolengwa kuwa matokeo ya mafunzo hayo: kuwawezesha vijana kuelewa vipaumbele vya majadiliano ya tabianchi na kujiandaa ipasavyo, kuwasilisha hoja zenye lengo la kuathiri maamuzi, kujenga ushirikiano na mitandao, pamoja na kutafsiri maarifa kuwa vitendo.

“Tunataka vijana wawe na taarifa sahihi na maandalizi ya kutosha, wajue namna ya kuwasilisha hoja zao ili kuathiri matokeo ya majadiliano, wajenge ushirikiano na mitandao, na zaidi ya yote, watumie maarifa kubadili maisha ya watu,” amesema.

Dk Kitogo amesema vijana 61 waliochaguliwa kushiriki mafunzo hayo walipatikana kwa kuzingatia sifa na juhudi zao katika kushiriki masuala ya mabadiliko ya tabianchi, akibainisha kuwa idadi hiyo ni sehemu ndogo tu ya vijana wengi wenye uwezo na utayari wa kuchangia katika ajenda hiyo.

Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Maendeleo ya Vijana, Bestina Gunje, amesema mafunzo hayo yanalenga kuhakikisha vijana wanashiriki kwa tija katika masuala ya tabianchi, ikiwemo mabadiliko ya kuelekea uchumi usiochafua mazingira na biashara ya hewa ukaa.

Amesema maandalizi kuelekea Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) yanapaswa kwenda sambamba na utekelezaji wa ahadi na maamuzi yanayofikiwa katika mikutano hiyo.

“Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine, inakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi. Wizara inaona umuhimu wa vijana kushiriki katika ajenda hizi muhimu ili waweze kuzungumzia maslahi ya nchi yetu na Afrika kwa ujumla,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Human Dignity and Environmental Care Foundation (HUDEFO), Sarah Pima, ambaye ni miongoni mwa waratibu wa programu hiyo, amesema ushiriki wa vijana ni muhimu katika kuongeza uwakilishi na sauti ya Afrika kwenye mikutano ya kimataifa.

Amesema miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa na kuingizwa katika azimio hilo ni kuanzishwa kwa mfuko wa kufadhili vijana wa Afrika wanaoshiriki katika masuala ya tabianchi, pamoja na changamoto mpya zinazohusiana na madini muhimu na biashara ya hewa ukaa.

Pima amesema masuala hayo yanahitaji kupewa kipaumbele ili vijana wa Afrika waweze kushiriki kikamilifu katika mijadala na maamuzi yanayohusu rasilimali na maendeleo ya bara hilo.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Deon Shekuza kutoka Namibia amesema ushiriki wa vijana ni muhimu katika kutekeleza ajenda za maendeleo za Afrika, ikiwemo Ajenda 2063, kwa kuwa vijana ndio watakaoishi na matokeo ya mikakati hiyo kwa muda mrefu.

Amesema ni muhimu kuhakikisha ajenda za mazingira na maendeleo zinazopewa kipaumbele zinaakisi mahitaji na maslahi ya Waafrika wenyewe.

“Ushiriki huu ni muhimu kwa manufaa ya Afrika. Tunaona kuwa wengi wanaotoa fedha za miradi si Waafrika, hivyo tunapaswa kujiuliza: tunapotekeleza miradi hiyo, tunahudumia ajenda za nani? Huu ni mwanzo mzuri wa kuanzisha mambo yanayotuhusu moja kwa moja,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Thamini Jamii Organization ya Zanzibar, Sabrina Soud, amesema anatarajia mafunzo hayo yataendelea na kuwa jukwaa la kudumu la kuwaunganisha vijana wa Afrika katika ajenda ya tabianchi.

Amesema ushirikiano huo unaweza kuwawezesha vijana kuwa na msimamo wa pamoja katika kusaidia serikali zao na bara la Afrika kutafuta suluhisho la changamoto zinazokabili jamii zao.

“Tunaweza kujenga pamoja na kuwa na sauti moja katika kusaidia serikali zetu na bara letu la Afrika kwa ustawi wa jamii zetu,” amesema.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *