Magonjwa yasiyoambukiza yaendelea kutishia maisha, wataalamu waonya
5 mins read

Magonjwa yasiyoambukiza yaendelea kutishia maisha, wataalamu waonya

Kibaha. Wataalamu wa afya wameonya kuhusu kuongezeka kwa hatari ya magonjwa yasiyoambukiza, yakiwamo magonjwa ya moyo, kiharusi, kisukari na kansa, wakisisitiza umuhimu wa kujikinga, kupima mapema na kupata matibabu kwa wakati.

Wamesema mtindo wa maisha, ikiwamo unywaji wa pombe, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, kuongeza chumvi kwenye chakula na kutofanya mazoezi, ni miongoni mwa vihatarishi vya magonjwa hayo.

Aidha, wameeleza kuwa gharama kubwa za matibabu ni mojawapo ya changamoto zinazowakabili wagonjwa, hivyo kuhimiza jamii kuchukua hatua za kinga kabla ya magonjwa hayo kusababisha madhara makubwa.

Akitoa elimu kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) mjini Kibaha, Mkoa wa Pwani, leo Jumatatu Oktoba 26, 2026, Dk Samwel Rweyemamu mbobezi wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), amesema magonjwa yasiyoambukiza yanahitaji hatua madhubuti za kuzuia na kudhibiti madhara yake.

Dk Rweyemamu amesema magonjwa yasiyoambukiza yanachangia asilimia 34 ya vifo vyote nchini, huku visababishi vingine vikichangia asilimia 66.

Ametaja magonjwa ya moyo, shinikizo la juu la damu, kiharusi, kansa, kisukari na magonjwa sugu ya mfumo wa upumuaji kuwa miongoni mwa changamoto kubwa za afya.

Amesema majeraha na ajali za barabarani pia ni miongoni mwa visababishi vikuu vya vifo nchini.

Akizungumzia ukubwa wa tatizo hilo duniani, Dk Rweyemamu amesema magonjwa ya moyo husababisha vifo vya watu zaidi ya milioni 8.99 kwa mwaka, huku shinikizo la juu la damu likihusishwa na vifo milioni 10.85 na kiharusi kikitajwa kufikia milioni 93.8 duniani.

Aidha, amesema watu milioni 612 duniani wanaishi na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.

Kisukari chatajwa kuwa tishio

Akizungumzia kisukari, Dk Rweyemamu amesema ugonjwa huo husababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 1.5 duniani kwa mwaka.

Amesema Tanzania ina zaidi ya watu milioni 3.5 wanaoishi na kisukari, huku vifo vinavyohusishwa na ugonjwa huo vikikadiriwa kufikia 44,000 kwa mwaka.

Daktari wa Magonjwa yatokanayo na kazi kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Elias Bilago akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), kuhusu elimu ya magonjwa hayo na hatua za kuchukua wakati wa Mkutano Mkuu wa Mamlaka hiyo uliofanyika leo Oktoba 26, 2026 Kibaha mkoani Pwani. Picha na Said Powa

Ameonya kuwa kisukari kisipodhibitiwa kinaweza kusababisha madhara makubwa, yakiwemo kuathiri moyo, kuharibu figo na kusababisha matatizo ya nguvu za kiume.

Ametaja pia kansa ya matiti ni miongoni mwa magonjwa yanayochangia vifo, akisisitiza umuhimu wa kutambua magonjwa hayo mapema ili wagonjwa wapate huduma stahiki kwa wakati.

Akieleza changamoto zinazokwamisha mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, amesema uhaba wa maeneo ya kufanyia mazoezi, mabadiliko ya maadili katika jamii, uelewa mdogo kuhusu vihatarishi na gharama kubwa za matibabu ni mambo yanayohitaji kushughulikiwa.

“Gharama za matibabu zipo juu sana. Kwa mfano, matibabu ya kansa hugharimu kati ya Sh5 milioni hadi Sh10 milioni kwa mwaka kwa mgonjwa mmoja,” amesema.

Mbali na magonjwa hayo, ametaja selimundu na matatizo ya afya ya akili kuwa miongoni mwa changamoto zinazoathiri jamii. Amesema matatizo ya afya ya akili yanaweza kuambatana na msongo wa mawazo na hali ya kuchanganyikiwa.

Homa ya ini na hatari ya saratani

Kwa upande wake, Dk Elias Birago mbobezi wa magonjwa yatokanayo na kazi, ameonya kuhusu maambukizi ya virusi vya homa ya ini, akieleza kuwa virusi vya hepatitis B vinaweza kusababisha madhara makubwa kwenye ini na kuongeza hatari ya kupata saratani ya kiungo hicho.

“Homa ya ini ni ugonjwa unaotokana na shambulizi kwenye ini na unaweza pia kuchangiwa na mambo mbalimbali, kama unywaji wa dawa bila kufuata taratibu za kitaalamu, ingawa kwa kiwango kikubwa husababishwa na virusi,” amesema.

Amesema ugonjwa huo unaweza kuanza kwa dalili zinazofanana na homa ya kawaida na baadaye kuwa mkali zaidi.

Ameeleza kuwa hepatitis B huambukizwa kupitia damu na majimaji mengine ya mwili, akitaja njia za maambukizi kuwa ni kuongezewa damu yenye virusi, kuchangia vifaa vyenye ncha kali, mama kumwambukiza mtoto wakati wa kujifungua, kuchangia miswaki na kujamiiana.

“Wanaohitaji kuongezewa damu, wanaojidunga dawa, wagonjwa wanaofanyiwa dialisis na wahudumu wa afya ni makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukizwa ugonjwa huu,” amesema.

Dk Birago amesema dalili za homa ya ini zinaweza kuwa homa, maumivu upande wa kulia wa tumbo, mkojo kuwa mweusi, uchovu na macho kuwa ya njano.

Hata hivyo, amesema mtu anaweza kuishi na maambukizi hayo kwa zaidi ya miaka 20 bila kuonyesha dalili, hali inayosisitiza umuhimu wa kupima ili kujua hali ya afya.

Amesema utambuzi wa ugonjwa huo hufanyika hospitalini kwa kutumia vipimo vya damu, uchunguzi wa utendaji wa ini na vipimo vya kupima wingi wa virusi vya hepatitis B (HBV).

“Njia za kujikinga na ugonjwa huu ni kuepuka ngono zembe, kuacha kuchangia vitu vyenye ncha kali, kupima na kupata chanjo ya kujikinga,” amesema.

Ameongeza kuwa mtu asiye na maambukizi anaweza kupata chanjo, huku aliyebainika kuwa na maambukizi akipatiwa ushauri na matibabu kulingana na hali yake.

Amesisitiza hatua tatu muhimu za kukabiliana na ugonjwa huo kuwa ni kupima ili kujua hali ya afya, kupata chanjo kwa wanaostahili na kuzuia maambukizi kwa kuepuka tabia hatarishi.

Serikali yaimarisha udhibiti

Wakati wataalamu hao wakisisitiza umuhimu wa kinga na matibabu ya mapema, Serikali inaendelea kuchukua hatua za kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza nchini.

Miongoni mwa hatua hizo ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza wa mwaka 2021–2026, unaolenga kuimarisha uratibu wa sekta mbalimbali, miundombinu ya huduma za afya, tafiti na uelewa wa umma kuhusu magonjwa hayo.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *