Wanawake waongoza mahafali ya kwanza TIA Zanzibar, Waziri Omar atoa neno
Unguja. Imeelezwa hatua kubwa imepigwa katika kufikia usawa wa jinsia kwenye elimu ya juu, ambapo wanawake wameweka historia kwa kuongoza idadi ya wahitimu katika mahafali ya kwanza ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Zanzibar.
Akizungumza akiwa mgeni rasmi leo Oktoba 28, 2026 katika mahafali ya 24 ya TIA lakini ya kwanza kwa Zanzibar, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amebainisha kuwa kati ya wahitimu 188 waliotunukiwa vyeti na shahada, wanawake ni 127 sawa na asilimia 68 huku wanaume wakiwa.
“Matokeo haya yanaashiria kuondoka kwa changamoto ya kihistoria ambapo idadi ya watoto wa kike ilikuwa ikipungua kwa kasi wanapopanda ngazi za elimu kutoka shule ya msingi na sekondari hadi elimu ya juu,” amesema Balozi Omar.
Amefafanua kuwa mambo matatu makuu katika elimu ni fursa, usawa na ubora akisisitiza kuwa matokeo haya yanadhihirisha kuwa fursa na usawa vimepatikana kikamilifu kwa watoto wa kike.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya TIA, Profesa William Pallangyo ameeleza kuwa wanawake wameonyesha mfano wa kuigwa na kushika hatamu katika ufaulu na idadi ya wahitimu.
Ameeleza kuwa hatua hii ni utekelezaji wa vitendo wa Dira ya Taifa 2050 inayosisitiza usawa wa kijinsia, uwekezaji kwa wanawake kama injini kuu ya maendeleo ya Taifa, na uandaaji wa viongozi wanawake wa kesho.
Mbali na usawa wa jinsia, Waziri wa Fedha ameeleza kuwa Kampasi ya Zanzibar ilianza mwaka 2023 ikiwa na wanafunzi 59, na sasa ina wanafunzi 267, huku malengo yakiwa ni kufikia wanafunzi 1,740 mara miundombinu itakapokamilika.
Kitaifa, chuo cha TIA kina zaidi ya wanafunzi 34,612 katika kampasi zake nane. Waziri amewapongeza wazazi waliojitoa kuwasomesha watoto wao.
Waziri Omar, amewasihi wahitimu hao katika mambo makuu matatu ikiwamo utiifu wa sheria, ubunifu wa teknolojia, uadilifu na weledi.
Mkuu wa taasisi alibainisha kuwa wahitimu 123 wametunukiwa Shahada ya Uzamili na 65 wametunukiwa vyeti vya ngazi mbalimbali, ambapo zaidi ya asilimia 70 ya wahitimu wa uzamili ni watumishi wa wizara na mashirika ya umma Zanzibar.
Amesema ongezeko la wanafunzi limesaidia kupunguza gharama za nauli na malazi kwa wanafunzi wa Zanzibar waliokuwa wakisafiri kwenda Tanzania Bara.
Hii inaendana na Dira ya Taifa 2020 inayohakikisha hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma kijiografia.
Profesa Palangyo amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inagharamia ujenzi wa kampasi ya kudumu katika eneo la hekari 60 lililotolewa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, huko Makunduchi Shehia ya Nganani.
Amesema awamu ya kwanza ina thamani ya Sh15.9 bilioni ambapo umefikia asilimia 45.
“Mradi huu unachochea uchumi wa buluu kwani asilimia 70 ya vibarua ni vijana wa eneo hilo na vifaa vinanunuliwa kwa wajasiriamali wa Zanzibar,” amesema
Pia, amesema wanafunzi 137 wamenufaika na mikopo ya ZHB, Chuo kimeingia ushirikiano wa kimataifa na vyuo vikuu vya Msumbiji na Chuo cha Mafunzo Zanzibar ili kuwajengea uwezo wafungwa katika ujasiriamali.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Fedha, Profesa Jehovaness Aikaeli amebainisha kuwa TIA imedhamiria kuwa kinara katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050, ambapo wahitimu watakuwa suluhu katika sekta ya umma na binafsi
Amesema Bodi imeridhishwa na ukuaji wa kampasi na mradi wa Makunduchi huku akitaja maeneo matatu makuu yanayozingatiwa na Bodi.
“Ubora wa taaluma na uchumi wa maarifa, utawala borana jumuishi na ukuaji endelevu na ushirikiano,” amesema
Wakizungumza kuhusu idadi kubwa ya wahitimu wanawake, baadhi ya wahitimu wamesema inatokana na jamii kubadili mtazamo na kuwasomesha watoto wa kike.
“Hii ni fursa kubwa wa sisi wanawake au wasichana kuongeza jitihada maana kwa sasa jamii imeanza kutambua umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike na kuondoa vikwazo,” amesema Aisha Hassan mmoja wa wahitimu.

