Waliohukumiwa maisha kwa kusafirisha heroini walivyoachiwa
4 mins read

Waliohukumiwa maisha kwa kusafirisha heroini walivyoachiwa

Arusha. Mahakama ya Rufani iemwaachia huru watu wawili Abdallah Chande na Crispin Francis, waliokuwa wamehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 7.73.

Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kubaini upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha uhusiano wao na dawa hizo za kulevya bila kuacha shaka.

Pia, walibaini upekuzi ulipelekea kupatikana dawa hizo haukufuata taratibu za kisheria, mashahidi muhimu hawakauitwa kutoa ushahidi, huku kukiwa na migongano katika melezo ya shahidi huru kuhusu mazingira ya upatikanaji wa dawa hizo na hati ya mashtaka ilikuwa na kasoro kwa kushindwa kubainisha dawa hizo zilivyosafirishwa.

Ilidaiwa Julai 20, 2023, Abdallah alipokea vifurushi 15 vya dawa hizo kutoka kwa watu ambao hawakutajwa kisha akamkabidhi Crispin aliyedaiwa kuzihifadhi katika nyumba iliyopo Mtaa wa Kitonga, Kimara Kilungule, Dar es Salaam kabla ya upekuzi katika nyumba hiyo na kukuta vifurushi tisa vilivyokuwa na dawa hizo.

Uamuzi uliobatilisha hukumu hiyo umetolewa Oktoba 29, 2026 na majaji watatu ambao ni Patricia Fikirini, Omar Othman Makungu na Eliezer Feleshi na nakala ya uamuzi huo kuwekwa kwenye tovuti ya Mahakama.

Jaji Fikirini amesema baada ya kupitia mwenendo na hoja za pande zote, wamebaini kuwa dawa hizo zilipatikana kupitia upekuzi ambao haukufuata utaratibu wa kisheria, huku ushahidi wa mashahidi ukiwa na tofauti na baadhi ya watu walioweza kutoa maelezo muhimu kuhusu eneo zilipokutwa dawa hizo kutokuitwa mahakamani.

Kuhusu upekuzi uliofanyika katika nyumba iliyodaiwa kuhusishwa na Crispin, majaji walibaini kuwa haukuwa wa dharura na haukufuata taratibu za kisheria.

“Kwa sababu hizo, tumeridhika kwamba huu haukuwa upekuzi wa dharura na kwamba utaratibu uliotakiwa wa upekuzi na ukamataji haukufuatwa. Kwa hiyo kielelezo cha saba na dawa zilizopatikana vilipatikana kinyume cha sheria,” amesema.

Amesema mahakama pia iliona kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kumhusisha Abdallah na vifurushi tisa vya heroini vilivyopatikana Kimara, licha ya madai kuwa alikuwa amevipokea vifurushi 15 na kumkabidhi Crispin.

Majaji hao pia wamesema kuwa madai ya Abdallah kukiri kupokea vifurushi vya dawa hizo hayakutosha kuthibitisha kuwa dawa zilizowasilishwa mahakamani ndizo alizozitaja katika kauli yake.

Mahakama hiyo ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi dhidi ya warufani bila kuacha shaka, hivyo hukumu ya kifungo cha maisha waliyokuwa wamepewa na Mahakama Kuu haikuwa sahihi.

Sababu nyingine iliyochangia kuwaachia huru ni kutokuitwa kwa mashahidi muhimu, akiwamo mmiliki wa nyumba na mfanyakazi wa ndani, ambao wangeweza kutoa maelezo kuhusu umiliki na mazingira ya kupatikana kwa dawa hizo.

Jaji Fikirini amesema walibaini kuwa ushahidi wa shahidi huru ulikuwa na tofauti na maelezo ya askari kuhusu mazingira ya upekuzi.

Kuhusu hati ya mashtaka, Mahakama iliona kuwa haikueleza kwa uwazi aina ya kitendo cha usafirishaji wa dawa za kulevya kilichodaiwa kufanywa na washtakiwa, hivyo hawakupewa taarifa ya kutosha kuhusu kosa walilotakiwa kujibu.

“Hatua hiyo haikutoa taarifa ya busara iliyohitajika kuwawezesha kujua kwa usahihi wa kutosha kesi waliyotakiwa kujibu.Hivyo kesi dhidi ya warufani haikuthibitishwa bila shaka yoyote inayoweza kutia mashaka,”

“Na kutiwa kwao hatiani hakuwezi kuendelea,tunakubali rufaa zao,kutengua hukumu na adhabu za kifungo cha maisha na kuamuru waachiliwe huru,isipokuwa kama wanashikiliwa kwa sababu nyingine halali ,”amesema.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi,Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi,Dar Es Salaam,upande wa mashtaka uliita mashahidi saba.

Shahidi wa kwanza, ambaye alikuwa mtaalamu wa maabara, alieleza kuwa alichunguza vifurushi tisa vilivyowasilishwa kwake na kubaini vilikuwa na dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilogramu 7.73.

Shahidi wa pili, alieleza kuhusu utaratibu wa kufunga na kuwasilisha vielelezo kwa ajili ya uchunguzi, huku shahidi wa tatu, akieleza namna vielelezo vilivyopokelewa na kuhifadhiwa.

 Shahidi wa nne, ambaye alikuwa miongoni mwa askari waliohusika na operesheni hiyo, alieleza kuhusu kukamatwa kwa washtakiwa, madai ya Abdallah kukiri kupokea vifurushi vya dawa hizo na madai kuwa Ochanda aliongoza polisi kwenda eneo vilipohifadhiwa.

Aidha shahidi wa tano,ambaye alikuwa shahidi huru aliyeshuhudia upekuzi uliofanyika katika eneo la nyumba ya Kimara na kuweka saini kwenye hati ya upekuzi na ukamataji.

Shahidi wa sita, alitoa ushahidi kuhusu ukamataji na upekuzi, huku shahidi wa saba akieleza kuhusu kushuhudia utaratibu wa kufunga vielelezo.

Kwa upande wa utetezi, Abdallah, aliyekuwa shahidi wa kwanza wa utetezi (DW1), alikana kuhusika na dawa hizo na kusema hamfahamu Crispin,akikana kuhusishwa na kielelezo cha dawa kilichowasilishwa mahakamani.

Kwa upande wake DW2, alikiri kukamatwa eneo la Kinondoni, lakini alikana kupelekwa Kimara, kuifahamu nyumba iliyodaiwa kukutwa na dawa hizo au kuwaongoza polisi kwenda kuzikamata.

Aidha alikana kuwa na uhusiano na mmiliki wa nyumba hiyo na kupinga madai kuwa alisaini hati ya upekuzi na ukamataji.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *